Abstract:
Tasinifu hii inayoitwa “Nafasi ya Fasihi katika Ufundishaji wa Lugha ya Pili kenye Muktadha wa Mtaala Unaoegemea katika Uwezo: Mfano wa Shule Teule Wilayani Rusizi, RWANDA" ina malengo mahususi mawili. Lengo la kwanza ni kutathimini ufaafu wa fasihi
katika ufundishaji wa lugha ya pili na utekelezaji wa mtaala unaoegemea katika uwezo kwa wanafunzi wa Kiswahili wa kidato cha tano. Lengo la pili ni kubainisha namna fasihi inavyoweza kutumika katika ufundishaji wa lugha ya pili na utekelezaji wa mtaala unaoegemea katika uwezo kwa wanafunzi wa Kiswahili wa kidato cha tano. Taarifa zilipatikana kwa njia ya mahojiano, ushuhudiaji, na mapitio ya maandiko. Sampuli
iligawanyika katika makundi mawili ambayo ni watu na kazi za fasihi. Sampuli ya watu ni
walimu na wanafunzi wa Kiswahili katika kidato cha tano katika shule za sekondari, ilhali sampuli ya kazi za fasihi ilihusishakazi tofauti za fasihi andishi na fasihi simulizi. Sampuli ilipatikana kwa mbinu ya sampuli lengwa. Uchambuzi wa data umeegemezwa katika nadharia
mbili ambazo ni Utambuzi na Maingiliano ya Tamaduni-Jamii. Matokeo ya utafiti uliofanyika
yanaonesha kwamba fasihi hujumuisha mifano bora ya kufundishia lugha ya pili. Hii ni
kutokana na hoja kwamba katika kazi za fasihi, inapatikana mifano ya kufundisha sarufi,
msamiati na stadi zote za lugha. Pia, Matokeo ya utafiti uliofanyika yamebaini kwamba fasihi hutoa mifano ya uwezo wa jumla na masuwala mtambuka ikiwemo thamani na mwenendo mwema. Pamoja na hayo, utafiti umebaini kwamba fasihi hufaa kwa kufundishia lugha ya pili kwa upande mmoja na kutekeleza mtaala unaoegemea katika uwezo kwa upande mwingine.
Mwisho, utafiti umeonesha namna ambavyo fasihi inavyoweza kutumiwa kama nyenzo ya kufundishia lugha ya pili na kutekeleza mtaala unaoegemea katika uwezo.