Abstract:
Tasnifu hii inajadili nafasi ya fasihi andishi katika ukuzaji wa stadi za mawasiliano: mfano wa
shule za sekondari teule wilayani Nyanza. Utafiti uliofanyika ulikusudia kutimiza malengo
mahususi mawili. Lengo la kwanza lilikuwa kutathmini nafasi ya fasihi andishi katika ukuzaji wa
stadi za mawasiliano katika shule za sekondari sekondari teule wilayani Nyanza. Lengo la pili
lilikuwa kuunda miongozo ya kutumia fasihi andishi katika ukuzaji wa stadi za mawasiliano
katika shule za sekondari teule wilayani Nyanza. Utafiti uliongozwa na Nadharia ya
Mawasiliano. Aidha, katika ukusanyaji wa data, utafiti ulitumia usaili, ushuhudiaji na
uchanganuzi matini. Wango la utafiti lilihusisha walimu wa Kiswahili na wanafunzi
wanaojifunza katika mchepuo wa LFK. Mbinu ya usampulishaji lengwa ilitumiwa ili kupata
sampuli ya walimu 9 na wanafunzi 93. Matokeo ya utafiti yameonesha kwamba fasihi andishi
ina nafasi kubwa katika ukuzaji wa stadi za mawasiliano katika lugha ya Kiswahili kwa
wanafunzi wa shule za sekondari teule wilayani Nyanza. Kwanza, fasihi inakuza uwezo wa
kuwasiliana. Pili, inakuza stadi za lugha kama kusoma, kuandika, kusikiliza na kuzungumza.
Tatu, inakuza stadi ya ujasiri. Nne, fasihi andishi inachangia katika kukuza utambuzi wa hisia
kwa wanafunzi. Hata hivyo, kwenye shule za sekondari teule wilayani Nyanza, walimu wa
Kiswahili wanakumbana na changamoto kama mtazamo finyu kuhusu stadi za mawasiliano na
tathmini zinazosisitiza zaidi stadi za kuandika na kusoma. Vilevile, kwenye shule teule kuna
changamoto ya muda usiotosha na mbinu za ufundishaji zisizofaa ambazo hutumiwa na walimu
kwa kukuza stadi za mawasiliano kupitia ufundishaji wa stadi za mawasiliano katika Kiswahili.
Zaidi ya hayo, utafiti umeunda miongozo ya kutumia fasihi andishi kukuza stadi za mawasiliano
katika shule za sekondari teule wilayani Nyanza. Miongozo hii inajikita katika utumiaji wa
mbinu ya mawasiliano ya mtu mmoja kwa mwingine, uumbaji wa mazingira salama ya
kujifunzia na uhusiano wenye msaada na usikilizaji kwa makini. Isitoshe, utafiti uliofanyika
umedhihirisha mfano wa namna ya kufundisha fasihi kwa kuegemea kwenye miongozo ya
utumizi wa fasihi andishi katika kukuza stadi za mawasiliano miongoni mwa wanafunzi.
Mwisho, utafiti umependekeza kwamba walimu wa fasihi andishi wanalazimika kufanya juu
chini ili kutumia mbinu za ufundishaji mabazo zinakuza stadi za mawasiliano katika lugha ya
Kiswahili. Hii ni kwa sababu mawasiliano fasha katika lugha hii yanaweza kuwaletea wanafunzi
manufaa tele.