Abstract:
Utafiti wetu ulilenga kuchunguza athari za kifonolojia za Kinyarwanda katika ujifunzaji wa
lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo, malengo mahususi ya utafiti yalikuwa mawili. Mosi, kubainisha
athari za kifonolojia za lugha ya Kinyarwanda katika ujifunzaji wa Kiswahili katika shule za
sekondari teule wilayani Bugesera, Rwanda. Pili, kubainisha mikakati ya kukabili athari za
kifonolojia za Kinyarwanda katika ujifunzaji wa Kiswahili katika shule za sekondari teule
wilayani Bugesera. Utafiti uliongozwa na Nadharia ya Uchanganuzi Linganuzi. Wango la utafiti
lilikuwa walimu wa Kiswahili na wanafunzi wa shule za sekondari teule wilayani Bugesera.
Sampuli ya utafiti ilikuwa walimu wa Kiswahili 7 na wanafunzi 76 ambao walichaguliwa kwa
kutumia usampulishaji lengwa. Mbinu za uchambuzi matini, ushuhudiaji na mahojiano
zilitumika kukusanya data za kitaamuli ambazo zilichanganuliwa na kuwasilishwa kwa
madondoo na maelezo. Matokeo ya utafiti yameonesha kuwa, kuna athari za kifonolojia katika
ujifunzaji wa Kiswahili katika shule za sekondari teule wilayani Bugesera. Athari hizo ni pamoja
na uchopekaji, udondoshaji, ubadilishaji wa fonimu na mpangilio mbaya wa mofimu katika
maneno. Vilevile, matokeo yamebainisha sababu za athari hizo. Sababu ya kwanza ni ukosefu wa
mafunzo ya kina ya fonetiki na fonolojia kwa wanafunzi. Pili, ni mazingira ya nyumbani na
shuleni ambapo Kinyarwanda kinatumika zaidi kuliko Kiswahili.Tatu, ni shule kutilia mkazo
zaidi ufundishaji wa sarufi na fasihi kuliko fonolojia. Isitoshe, matokeo ya utafiti yamebainisha
mikakati ya kukabili athari hizo. Mikakati iliyotolewa ni pamoja na kulinganisha fonolojia ya
Kinyarwanda na ya Kiswahili, kutoa mazoezi ya kutosha yanayohusiana na fonolojia ya
Kiswahili na kuanzisha klabu za Kiswahili katika shule. Kwa hivyo, utafiti ulipendekeza
ushirikiano baina ya wanafunzi, walimu na viongozi wa shule ili kuondoa athari za kifonolojia za
Kinyarwanda katika ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili.