Abstract:
Utafiti husika wenye anwani, “Changamoto za Ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili
katika Shule za Ufundi Nchini Rwanda: Mfano wa Shule za Ufundi Wilayani Karongi”
ulilenga kutimiza malengo mahususi mawili ambayo ni kuchunguza changamoto
ambazo zinakabili ufundishaji na ujifunzaji wa lugha wa Kiswahili na pia kupendekeza
mikakati ya kukabili changamoto ambazo zinakabili ujifunzaji na ufundishaji wa
Kiswahili kwa wajifunzaji wa shule sekondari za ufundi wilayani Karongi. Ili
kukamilisha malengo haya, data za msingi na data za upili zilikusanywa kwa kutumia
mbinu ya ushuhudiaji, uchanganuzi matini na usaili. Wango la utafiti huu lilikuwa
wanafunzi wa madarasa ya Kiswahili, walimu wa Kiswahili na viongozi wa masomo
wa shule za sekondari za ufundi kwenye Wilaya ya Karongi. Sampuli ya utafiti
ilipatikana kwa kutumia mbinu ya sampuli lengwa. Utafiti wetu ulitumia mkabala wa
kitaamuli. Uchanganuzi na ufasiri wa data uliegemezwa kwenye Nadharia ya Utabia.
Licha ya tafiti kadhaa kuonesha kuwa Kiswahili ni lugha muhimu, matokeo ya utafiti
wetu yameonesha kwamba kuna changamoto ambazo zinakabili ufundishaji na
ujifunzaji wa lugha ya Kiswahili kwenye shule za sekondari za ufundi kwenye Wilaya
ya Karongi. Hii inatokana na ukosefu wa walimu wenye uwezo, ukosefu wa vifaa na
zana za kufundishia Kiswahili, muda usiotosheleza ufundishaji na ujifunzaji wa somo la
Kiswahili na ukosefu wa msukumo binafsi wa kujifunza Kiswahili miongoni mwa
wanafunzi. Ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na changamoto hizo, matokeo ya utafiti
yamebainisha mambo yanayoweza kushiriki katika uimarishaji wa ujifunzaji pamoja na
ufundishaji wa lugha ya Kiswahili. Mambo hayo yanasisistizia maandalizi ya mafunzo
na warsha kwa walimu wa Kiswahili, utumiaji wa vifaa vya TEHAMA, utengenezaji na
ufaraguzi wa zana za kufundishia Kiswahili na ukuzaji wa motisha ya kujifunza
Kiswahili miongoni mwa wanafunzi. Aidha, matokeo ya utafiti yamebainisha mikakati
ya kukabili changamoto ambazo zinakabili walimu wanapofundisha lugha ya Kiswahili.
Mikakati hiyo ni pamoja na: utumiaji wa mbinu ya ujifunzaji wa lugha kwa ushirikiano,
utumiaji wa mbinu ya ujifunzaji lugha kijumuia na utumiaji wa mbinu ya ujifunzaji wa
lugha unoegemea katika uwezo. Mwisho, utafiti huu umependekeza kuwa watu
wanaohusika katika elimu kwenye nchi ya Rwanda, wanalazimika kuungana mkono ili
kuitia jeki ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili kwenye shule za sekondari za ufundi
nchini Rwanda.