Abstract:
Tasnifu hii imetokana na utafiti uliokusudia kuchunguza Ukuzaji wa Tafakuri
Bunifu Kupitia Ufundishaji wa Fasihi kwa Wanafunzi wa Kiswahili, Shule
Teule za Sekondari Wilayani Kicukiro. Utafiti ulikuwa na malengo mahususi
mawili: kubainisha nafasi ya fasihi andishi ya Kiswahili katika ukuzaji wa
tafakuri bunifu miongoni mwa wanafunzi katika shule za sekondari nchini
Rwanda, na pia kuunda mwongozo wa ufundishaji wa tafakuri bunifu kupitia
fasihi miongoni mwa wanafunzi katika shule za sekondari nchini Rwanda. Ili
kukamilisha malengo haya mahususi, data za msingi na data za upili
zilikusanywa kwa kutumia mbinu ya ushuhudiaji, uchanganuzi matini na
usaili. Wango la utafiti huu lilikuwa walimu wa Kiswahili na wakuu wa
masomo walioteuliwa katika shule za sekondari Wilayani Kicukiro. Sampuli
ya utafiti ilipatikana kwa kutumia mbinu ya usampulishaji lengwa. Aidha,
utafiti ulitumia mkabala wa kitaamuli. Uchanganuzi na ufasiri wa data
uliegemezwa kwenye Nadharia ya Utambuzi. Licha ya matokeo ya utafiti
kuonesha kuwa fasihi ina nafasi muhimu katika ufundishaji wa tafakuri
bunifu, ilionekana kuwa baadhi ya walimu hawafanikiwi kujumuisha stadi ya
tafakuri bunifu sio tu katika maandalio ya masomo, bali pia katika
ufundishaji na tathmini. Hii inatokana na sababu zifuatazo: Walimu
kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu ufundishaji wa stadi za tafakuri
bunifu na utekelezaji wa MUU, muda mfupi wa kuandaa kazi za ufundishaji
na majukumu mengi ambayo walimu wanapaswa kutimiza. Ili kukabiliana na
vikwazo hivyo, matokeo ya utafiti yamebainisha mwongozo unaopaswa
kufuatwa na walimu katika ufundishaji wa stadi za tafakuri bunifu kupitia
fasihi. Mwongozo huu unaweka mkazo katika utumizi wa: kazi za makundi,
kazi za uigizaji, kazi za fikiri-jozi-changia na midahalo. Aidha, matokeo ya
utafiti yamebainisha mikakati tofauti inayoweza kutumiwa na walimu wa
fasihi ili kuimarisha stadi za tafakuri bunifu miongoni mwa wanafunzi.
Mikakati hiyo ni pamoja na utumiaji wa michezo ya maneno, maswali
bunifu, kazi wazi, hadithi duara na matumizi ya maswali ya mafumbo.
Mwisho, tasnifu hii imedhihirisha mfano wa namna ya kufundisha fasihi kwa
kuegemea katika mwongozo wa utumizi wa fasihi katika kukuza tafakuri
bunifu. Aidha, tasnifu hii inapendekeza kwamba wadau wote wa sekta ya
elimu wanalazimika kuungana mkono ili kuimarisha ufundishaji wa stadi za
tafakuri bunifu na stadi nyingine za karne ya ishirini na moja miongoni mwa
wanafunzi.