Abstract:
Utafiti huu ulikuwa na lengo kuu la kuchunguza ufundishaji na ujifunzaji wa stadi za kusoma na kuandika katika MUU kwa wanafunzi wa shule za upili kwenye wilaya ya Nyamagabe nchini Rwanda. Utafiti wetu ulikusudia kukamilisha malengo mahususi matatu yaliyokuwa ni pamoja na kubainisha namna ufundishaji na ujifunzaji wa stadi za kusoma na kuandika unavyofanyika kwa shule za sekondari kwenye wilaya ya Nyamagabe, kueleza changamoto za utekelezaji wa ufundishaji na ujifunzaji wa stadi za kusoma na kuandika katika utekelezaji wa MUU kwa shule za sekondari kwenye wilaya ya Nyamagabe na kupendekeza mikakati inayoweza kutumiwa na walimu katika ufundishaji wa stadi za kusoma na kuandika kupitia MUU kwa wanafunzi wa shule za sekondari kwenye wilaya ya Nyamagabe. Ili kutimiza malengo ya utafiti, utafiti wetu ulikusanya data kupitia mbinu ya usaili na uchanganuzi matini. Wango katika utafiti huu lilihusisha wakuu wa masomo pamoja na walimu wanaofundisha Kiswahili ambao walichaguliwa kutoka kwenye shule teule za sekondari za wilaya ya Nyamagabe kwa kutumia usampulishaji lengwa. Utafiti huu ulitumia mkabala wa kitamuli. Uchanganuzi wa data pamoja na ufasiri wa data uliongozwa na Nadharia ya Utamadunijamii. Aidha, matokeo ya utafiti wetu yalionesha kwamba walimu wanaofundisha Kiswahili kwenye wilaya ya Nyamagabe hawafundishi stadi ya kusoma na kuandika Kiswahili vilivyo kutokana na utumiaji wa mbinu za ufundishaji na ujifunzaji zisizofaa na ukosefu wa uwezo wa kuandaa vilivyo maandalio ya mafunzo yanayolenga kukuza uwezo wa usomaji na uandishi wa Kiswahili kwa wanafunzi. Baada ya matokeo ya utafiti kudhihirisha changamoto zinazokabili walimu wanapofundisha kuandika pamoja na kusoma Kiswahili katika utekelezaji wa MUU kwa shule za sekondari wilayani Nyamagabe ambazo ni ukosefu wa utamaduni wa kuandika na kusoma, upatikanaji na ufanisi wa vifaa vinavyohitajika katika kusoma na kuandika Kiswahili, ukosefu wa motisha miongoni mwa wanafunzi na uhaba wa walimu wa Kiswahili wenye uwezo, utafiti wetu umependekeza mikakati ambayo walimu wanaweza kutumia na walimu wanapofundisha stadi za kusoma na kuandika Kiswahili ili kuepuka changamoto zinazokabili walimu wanapofundisha kusoma na kuandika Kiswahili kwa wanafunzi wa shule za sekondari wilayani Nyamagabe. Mikakati hiyo ni utumiaji wa TEHAMA, utumiaji wa Andaa- Shiriki na Tafakari, utumiaji wa usomaji na uandikaji gawizwa na utumiaji wa mbinu ya ujenzi wa maarifa. Isitoshe, tasnifu hii inapendekeza kuwa ni lazima walimu, wakuu wa masomo, viongozi wa shule na wadau wengine wa sekta ya elimu waungane mkono kwa madhumuni ya kuimarisha shughuli za ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili kwenye ngazi zote za elimu katika nchi ya Rwanda.