Abstract:
Utafiti huu ulilenga kutathimini nafasi ya ufundishaji na ujifunzaji katika uimarishaji
wa Kiswahili kama lugha rasmi nchini Rwanda. Hii inatokana na Kiswahili kufanywa
kuwa lugha rasmi nchini Rwanda tangu mwaka 2017 Kwa hiyo, kwanza, utafiti huu
ulikuwa na malengo mawili: Kwanza, kubainisha nafasi ya ufundishaji na ujifunzaji
katika uimarishaji wa Kiswahili kama lugha rasmi nchini Rwanda. Pili, kujadili
vikwazo vinavyokabili ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili kama lugha rasmi nchini
Rwanda pamoja na kupendekeza suluhu. Nadharia ya Mwingiliano wa Kijamii ndiyo
iliyoongoza utafiti huu ambao ulikuwa wa kitaamuli. Walengwa wa utafiti husika
walikuwa wanafunzi wa madarasa ya Kiswahili, walimu wa Kiswahili, wakurugenzi na
viongozi wa Kiswahili katika taasisi tofauti nchini Rwanda. Sampuli ya wanafunzi 30,
walimu 3, wakurugenzi 3 na viongozi wa Kiswahili 3 ilipatikana kwa kutumia
usampulishaji lengwa. Ukusanyaji wa data ulitumia mbinu mbili ambazo ni usaili na
uchanganuzi matini. Data za kitaamuli zilizokusanywa, ziliwasilishwa na
kuchanganuliwa kwa kutumia madondoo na maelezo. Aidha, Matokeo ya utafiti
yameonesha kuwa ufundishaji na ujifunzaji una mchango mkubwa katika uimarishaji
wa Kiswahili kama lugha rasmi nchini Rwanda. Hii ni kwa sababu ufundishaji na
ujifunzaji unakuza siyo tu stadi, msamiati na ufahamu wa sheria za sarufi ya Kiswahili
bali pia unatoa mahali mwafaka pa kuzungumzia lugha ya Kiswahili. Vilevile, matokeo
ya utafiti yameonesha kwamba kuna vikwazo kadhaa vinavyokabili walimu
wanapofundisha Kiswahili katika shule za sekondari nchini Rwanda. Vikwazo hivyo ni
pamoja na mwingiliano wa lugha, ukosefu wa vifaa vya kuelimishia na kusomea
Kiswahili, uhaba wa walimu wenye ujuzi na uwezo wa kufundisha Kiswahili na
mtazamo hasi wa wanafunzi kuhusu lugha ya Kiswahili. Isitoshe, baada ya kudhihirisha
vikwazo, utafiti ulioibua tasinifu hii umependekeza suluhu za vikwazo vinavyokabili
walimu wanapofundisha Kiswahili katika shule za sekondari nchini Rwanda. Suluhu
hizo ni pamoja na matumizi ya mazoezi mengi ya mazungumzo, utumiaji wa vifaa vya
kiteknolojia, kuimarisha na kuendeleza mafunzo kwa walimu wa Kiswahili na kuondoa
mtazamo hasi kuhusu Kiswahili.