Abstract:
Tasnifu hii ni matokeo ya utafiti wenye anwani “Nafasi ya Fasihi Simulizi katika Ufundishaji na Ujifunzaji wa Stadi za Kusikiliza na Kuzungumza Kiswahili: Mfano wa Shule Teule za Sekondari Wilayani Nyagatare,” ambao ulikuwa na lengo kuu la kuchunguza nafasi ya fasihi simulizi katika kufundisha na kujifunza stadi za kusikiliza na kuzungumza. Malengo mahsusi yalikuwa kubainisha nafasi ya fasihi simulizi kufundishia na kujifunzia stadi za kusikiliza na kuzungumza, na kuunda mwongozo wa kutumia fasihi simulizi kufundishia na kujifunzia stadi
hizo. Ukusanyaji wa data ulifanywa kwa ushuhudiaji, mahojiano na uchanganuzi wa matini. Walengwa wa utafiti huu walikuwa wanafunzi na walimu wa Kiswahili katika shule mbili za Wilaya ya Nyagatare. Data zilizokusanywa zilichambuliwa kwa njia ya maelezo. Nadharia ya Utambuzi ndiyo iliyoongoza utafiti huu. Matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa fasihi simulizi ina nafasi muhimu katika ufundishaji na ujifunzaji wa stadi za kusikiliza na kuzungumza. Fasihi simulizi inawavutia wanafunzi, wakawa na motisha ya kujifunza bila uchovu. Hii inatokana na kuwa fasihi simulizi hutumia miktadha anuwai ya maisha ya kila siku na misamiati rahisi inayowawezesha wanafunzi kuelewa na kuzingatia usikilizaji na uzungumzaji. Kutokana na haya, mwongozo wa kutumia fasihi simulizi kufundishia stadi za kusikiliza na kuzungumza uliundwa, ili kuwaongoza walimu kufundisha stadi hizi. Mwongozo huu, unawasilisha mambo ya kuzingatia kwa kila hatua ya somo, kuanzia mandalizi ya somo, utoaji wa somo na tathmini. Mapendekezo mbalimbali yametolewa kwa wadau mbalimbali, ili kufanikisha uungaji mkono na kutiliwa maanani kwa ufundishaji na ujifunzaji wa stadi za kusikiliza na kuzungumza kama stadi za msingi.